Tahajia

Ikiwa mtu anasoma taarifa ya habari katika mtandao na anakumbana na uandikaji mbovu wa maneno huenda akajiuliza: “Ikiwa mwandishi hakuchukua hadhari katika uandishi wake, kwa nini nimuamini?”

Kujifunza tahajia yaani kuendeleza maneno au uandikaji wa maneno sawasawa ni muhimu kwa sababu uwezo wa kuandika maneno sawasawa unamsaidia sana mtu katika maisha.  Ni muhimu kama uwezo wa kuandika na wa kusoma.

Kwa hakika, kuweza kuandika maneno sawasawa kunawasaidia watoto — na hata watu wazima — kuongeza uwezo wao wa kusoma na kuandika vyema.  Na hili ni muhimu kwa maendeleo ya watu na hata ya taifa.

Hamna shaka yoyote kwamba kipindi kizuri cha mtu kujifunza kuandika maneno sawasawa ni utotoni mwake. Lakini utashangaa kwamba kuna idadi kubwa ya watu wazima wasioweza kuandika sawasawa. Na hili linazidi kuwa tatizo kwa kuzuka majukwaa mepya ya mawasiliano ya kisasa ikiwa pamoja na mitandao ya habari, mablogi na uwezo wa kupelekeana na kupokea kwa simu jumbe fupi za maandishi, Facebook, twitter na hata katika maandishi ya baruapepe.

Kuna wenye kuamini kwamba watu wanaoandika kwenye majukwaa ya mawasiliano wanafupisha mambo wanayoyaandika kwa kuondosha baadhi ya herufi au kwa kuchanganya nambari na herufi.  Hivyo, wanahoji kwamba maandishi kama hayo ambayo yana tahajia mbovu yanaiathiri lugha na hasa namna inavyoandikwa.

Wengine hawakubali lakini namna Kiswahili kinavyoandikwa siku hizi ni ushahidi wa kutosha kwamba mawasiliano ya kisasa yameathiri vibaya tahajia. Hayo ni matokeo na matokeo hayo nayo huwa na matokeo mengine.  Nayo ni kwamba watu wanakuwa hawaoni taabu kuukimbia mtandao wako wa habari iwapo wataona kwamba unafanya makosa ya tahajia.

Hoja watayoitoa inafahamika. Watasema: “Kwa nini tuuamini mtandao huu ikiwa unashindwa hata kuandika sawa, kwa tahajia sahihi?”

Tahajia inakuwa haina umuhimu wowote tunapozungumza, lakini tunapoandika, tahajia huwa na umuhimu mkubwa. Ulimwengu wa leo umejaa maandishi. Siku hizi kuna jumbe fupi za maandishi kwenye simu (sms), baruapepe, majukwaa ya kijamii, na mitandao ya habari ya watu binafsi au ya vikundi vya watu.

Mote humo mnatumiwa maneno. Na ni muhimu maneno yanayotumiwa hasa katika mitandao ya habari yaonekana kuwa yako sawa kama ilivyo muhimu kwa namna yanavyosikika. Ikiwa mtu anasoma taarifa ya habari katika mtandao na anakumbana na uandikaji mbovu wa maneno huenda akajiuliza: “Ikiwa mwandishi hakuchukua hadhari katika uandishi wake, kwa nini nimuamini?”

Kwa ufupi, makosa ya tahajia katika mitandao ya habari yanawaudhi sana watu kiasi cha kuwafanya waache kuizuru mitandao hiyo.  Kwa hivyo, kuna kila uwezekano kwamba watu wataanza kuuhama mtandao wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, kwa mfano, iwapo wataona kwamba BBC inafanya makosa ya tahajia katika mtandao wake. Wasomaji wa mtandao huo wanaweza wakavunjika moyo na wasiuzuru tena mtandao huo.

Halafu kuna suala la uhalali wa maandishi yaliyo kwenye mtandao wa habari kama wa BBC. Tahajia mbovu yaani uandikaji mbovu wa maneno kwenye mtandao unamfanya msomaji awe na wasiwasi na uhalali wa yale anayoyasoma na pia autilie shaka mtandao wenye maandishi hayo. Huwa hawezi kuyaamini wala kuuamini mtandao.

Jambo jengine ni kwamba uandikaji mbovu wa maneno huenda ukamfanya msomaji ahisi kwamba aliyeandika hamheshimu au kwamba mtandao ulio na maandishi hayo ni mtandao ovyo usio na maana ambao haupaswi kuheshimiwa au kutiwa maanani.

Hii hapa mifano miwili ya tahajia mbovu:

  1. “Mkuu wa Chama cha Wachimba migodi alihutubia kwa khadhabu kuhusu shida wanazopata wachimba migodi.” (Tahajia iliyo sahihi ni: ghadhabu.)
  2. “Hata hivyo nchi hiyo imeweza kugeuka kuwa moja ya mataifa yanayokuwa kwa kasi kubwa barani Afrika. (Tahajia iliyo sahihi ni: yanayokua

Saini ya mfanyakazi

Subiri, tuhakikishe ikiwa unahusika na mtandao wa kazini wa BBC

Samahani, hatukuweza kuthibitisha kuwa wewe ni mfanyakazi wa BBC

  • Tafadhali hakikisha umo katika mtandao wa kazini wa BBC
  • Tafadhali hakikisha kiungo unachojaribu kufikia ni  sahihi
Funga na uendelee

Umekubalika katika mtandao wa BBC

Funga na uendelee