Kipindi cha kuzungumza kwa simu

Ukiuliza swali linalohitaji jibu la “ndio” au “hapana" inakupasa utazamie jibu fupi … na katika hali hiyo basi itakubidi uulize “kwa nini?” … na mazungumzo yataendelea.

Na mtangazaji wa BBC Julian Worricker

Siri ya kufanikisha kipindi cha kuzungumza kwa simu ni kuwa na mada na swali linalofaa.

Swali linapaswa liwe fupi, wazi na, kinyume na jinsi ilivyofunzwa zamani katika vyuo vya utangazaji, pengine linahitaji jibu la “ndio” au “hapana.”

Mifano mizuri ya maswali hayo ni kama lile liloulizwa wakati wa waziri mkuu wa zamani wa Uingereza: “Je, ni wakati wa Gordon Brown kun’agtuka?”. Au “Jee vita dhidi ya ugaidi vinafanikiwa?” Maswali hayo hayakuzuii wewe mtangazaji kuuliza maswali ya ziada ya watu wanaopiga simu wala kuzungumzia mambo mengine ikiwa wasikilizaji wanakuelekeza upande huo. Lakini maswali hayo yanakufanya wewe na wale wanaochangia kukazia fikira mada inayozungumziwa.

Ukiuliza swali linalohitaji jibu la “ndio” au “hapana” inakupasa utazamie jibu fupi … na katika hali hiyo basi itakubidi uulize “kwa nini?” … na mazungumzo yataendelea.

Kupanua wazo

Baada ya kuuliza swali fupi, la wazi – utafanya nini ili uamshe hamu ya wasikilizaji wako? Unaweza kutumia habari za ziada:

“Je, ni wakati wa Gordon Brown kung’atuka?”

... uliza. Halafu ...

“Kuna taarifa katika gazeti la leo la Daily Telegraph kuwa waziri fulani wa cheo cha juu amesisitiza Bw Brown ajiuzulu kabla ya mwisho wa mwaka huu. Ikiwa watu walio karibu naye wameacha kumuunga mkono, je, anaweza kubaki mamlakani? Je, anakisaidia chama chake na nchi hii kwa kubaki mamlakani? Au unafikiria anapaswa kuwapuuza wachambuzi na kuendelea kukaa Downing Street kama apendavyo? Ndiyo sababu tunauliza, je, ni wakati wa Gordon Brown kung’atuka?”

Hivyo basi umewapa wasikilizaji maelezo au habari zaidi zitakazowachochea kupiga simu, lakini bado umewakumbusha swali kuu.

“Tafadhali piga simu”

Katika mfano huo, labda nukuu fulani la mchambuzi au mtu anayemuunga mkono Gordon linaweza kusaidia kuchochea mazungumzo hayo. Hiyo ni mbinu ya kupata simu nyingi. Unachosema ni “tafadhali piga simu,” lakini unafanya hivyo kwa ustadi.

Bila shaka, itakuwa afadhali zaidi ukipata nafasi ya kufanya hivyo katika kipindi kinachotangulia chako. Mara nyingi ni vigumu kupata simu ya kwanza. Na usione haya kurudia nambari ya simu mara kadhaa.

Mpigaji simu wa kwanza: peperusha simu yake hewani haraka iwezekanavyo. Kulingana na kanuni moja kuhusu vipindi vya kuzungumza kwa simu, “mtu mmoja akipiga simu, wengine watapiga simu”. Watu wengi wanahitaji ujasiri ili wapige simu – lakini wakishasikia wengine wakifanya hivyo watachochewa kufanya hivyo pia.

Hata ikiwa yule anayepiga simu hatimizi matarajio yako, simu yake ni afadhali kuliko kutopata simu yoyote. Kwa hivyo, chukua simu yake na uipeperushe hewani. Na ikiwa una wageni watakaojibu swali la kwanza, usiwaalike kufanya hivyo wakati huo.

Ikiwa mpigaji simu anasubiri kuzungumza, chukua simu yake kwanza … kisha waalike wageni wachangie.

Vipindi vya Kuzungumza kwa Simu: Wageni: na mtangazaji wa BBC Julian Worricker

Ukiwa na wageni mbalimbali wakati wa kipindi cha kuzungumza kwa simu, kipindi hicho kitapendeza na kuwatia watu hamu ya kusikiliza.

Kuna wakati ambapo wageni wawili walipachikwa katika studio na ilikuwa rahisi kutabiri wangekuwa na maoni tofauti kuhusu mada inayozungumziwa. Huenda mbinu hiyo bado ikafanikiwa katika hali fulani, lakini mada nyingi zinaweza kuzungumziwa kwa njia nyingi kuliko kupata tu maoni ya pande mbili.

Kwa hiyo, panga mgeni mmoja awepo kwa dakika 20 za kwanza, kisha mweke kando na umhusishe mwingine. Husisha mmoja tu kwa muda fulani, au ukipenda usimhusishe yeyote. Kisha wahusishe watatu.

Uzuri ni kwamba hakuna sheria kali kuhusu jambo hilo. Kumhusisha mgeni mwingine kunaweza kuwasaidia wapigaji simu kupata mtazamo tofauti.

Fanya hivyo baada ya mazungumzo kuendelea kwa nusu saa, na huenda utapata simu kutoka kwa watu wengine tofauti.

Kuwajaribu wapigaji simu

Hapa tunazungumzia hali ya sauti – kadiri unavyopata uzoefu katika vipindi vya kuzungumza kwa simu ndivyo wasikilizaji watakavyokuzoea na kufahamu mtindo wako.

Wapigaji simu hawapaswi kwenda hewani wakitarajia kwamba watasema watakayo bila kusahihishwa. Lakini pia wao si wanasiasa, kwa hiyo wasishambuliwe vikali kama wale wanaofanya maamuzi.

Hata hivyo, hakuna sheria, acha mazungumzo yawe ya kawaida. Watu fulani wanaopiga simu hufurahia kushambuliwa; wengine huogopa kuulizwa-ulizwa maswali. Hata ufanye nini, hutafanya mambo kikamilifu.

Pasina budi utawakasirisha watu kadhaa, na unapaswa kuwa tayari kupatwa na matokeo ya jambo hilo. Huenda pia ukachambuliwa kwa kuwaruhusu watu kusema mengi mno bila ya uthibitisho. Huwezi kujua kila kitu nawe huhitaji kujua kila kitu ili kuwauliza wapigaji simu maswali.

Lakini uwe na hakika kwamba mtu fulani anayepiga simu anajua jambo fulani usilojua. Na katika enzi hizi ambapo ni rahisi kupata habari, muda si muda, atakueleza jambo hilo. Hilo litasawazisha mambo.

Tarajia Yasiyoepukika

Umekwisha soma hoja zako, umefanya utafiti, umekwisha fikiria hoja zitakazozushwa – kisha mtu fulani anapiga simu na kumtukana au kumtupia vijembe mwingine, au anakuchokoza. Hilo litatukia.

Tayarisha jinsi utakavyojibu. Mtu akimvunjia heshima mwenzake, ingilia kati na kusema: “Ni wazi kwamba Bwana X hayupo ili kujibu shutuma hizo, wala hatuna njia ya kubaini ikiwa usemayo ni kweli. Hivyo basi, nitakuruhusu utuage ili kipindi kiendelee.”

Ikiwa unaendesha mitambo, basi unaweza kumzima mpigaji simu huyo pole kwa pole; ikiwa mitambo inaendeshwa na fundi wa mitambo basi atahitaji kufanya hivyo mwenyewe.

Mtu akitupa vijembe, ingilia kati na kusema: “Samahani kukukatiza lakini inafaa utambue kwamba mambo uliyosema huenda yakawakasirisha wasikilizaji fulani. Basi nitachukua simu nyingine.”

Unapaswa kuwaomba radhi wasikilizaji. Kwa maoni yao, wamesikia mambo machafu kupitia idhaa ya BBC. Jikumbushe Sera za Uhariri za BBC kuhusu lugha chafu; na pia jinsi ya kushughulikia hali ngumu wakati wa kupeperusha matangazo ya moja kwa moja.

Jitahidi usivurugwe na mambo yasiyotarajiwa. Usipobabaishwa na tukio hilo, wasikilizaji hawatalikazia fikira sana na mazungumzo yataendelea.

Usiposhughulikia hali hiyo kwa njia inayofaa, mazungumzo yatakosa hadhi yake na yanaweza kuvurugwa kabisa

Saini ya mfanyakazi

Subiri, tuhakikishe ikiwa unahusika na mtandao wa kazini wa BBC

Samahani, hatukuweza kuthibitisha kuwa wewe ni mfanyakazi wa BBC

  • Tafadhali hakikisha umo katika mtandao wa kazini wa BBC
  • Tafadhali hakikisha kiungo unachojaribu kufikia ni sahihi
Funga na uendelee

Umekubalika katika mtandao wa BBC

Funga na uendelee