|
Kikwete aongoza maoni Tanzania | |||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ameongoza kura za maoni ya wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC katika kuwania tikiti ya CCM kwenye uchaguzi wa rais nchini humo. Kikwete ambaye alianza kwa kasi ndogo, alimaliza fainali akiwa na kura 3161 ambazo ni sawa na asilimia 48.2. Dr Salim Ahmed Salim, aliyewahi kuwa katibu mkuu wa OAU amekuwa wa pili baada ya kupigiwa kura 1963 sawa na asilimia 29.9. Katika nafasi ya tatu yupo waziri mkuu wa sasa Frederick Tluway Sumaye aliyekusanya kura 418 kiulinganifu sawa na asilimia 6.6. Wagombea wengine Makamu mwenyekiti wa CCM, John Samwel Malecela amekuwa wa nne kwa kuweka kibindoni kura 320 au asilimia 4.8 na waziri wa mawasiliano Professor Mark James Mwandosya amekuwa wa tano kwa kufikisha kura 265 sawa na asilimia 4.0. Wanasiasa hao watano ni kati ya karibu 12 wa CCM waliohusishwa katika kura hiyo ya maoni, ambayo ilipokea jumla ya kura 6555 zilizopigwa na wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC kwa kutumia ujumbe mfupi kwa njia ya simu. Msimamo wa matokeo 1.Jakaya Mrisho Kikwete - 3161 [ Asilimia 48.2] 2.Dr Salim Ahmed Salim - 1963 [ Asilimia 29.9] 3.Frederick Tluway Sumaye - 418 [ Asilimia 6.6] 4.John Samwel Malecela - 320 [ Asilimia 4.8] 5.Prof Mark James Mwandosya - 265 [ Asilimia 4.0] 6.Getrude Mongela - 120 7.John Pombe Magufuli - 62 8.Patrick Chokala - 60 9.Joseph Sinde Warioba - 47 10.Dr Ali Mohamed Shein - 45 11.Idd Simba - 30 12.Dr Abdallah Kigoda - 25 13.Dr William Shija - 20 Teknolojia Akitangaza matokeo hayo mkuu wa Idhaa ya Kiswahili, Tido Mhando, alisema kuwa kuwa maendeleo ya teknolojia yamewezesha kufanyika kwa kura hiyo jambo ambalo limeweza kuwashirikisha raia wa Tanzania wa aina zote. "Kwa kuwa hivi sasa karibu kila pembe ya dunia kwa swala hili, kila mahala Tanzania watu wanazo simu za mkononi, tunadhani tumeweza kupata maoni ya wa-Tanzania wa kila mahali na wa kila aina", alieleza Bw.Mhando. Akifafanua zaidi, Bw. Mhando alisema, “Watanzania wengi wameweza kushiriki labda kuliko kura yoyote nyingine ya maoni iliyokwisha kufanywa kuhusu uchaguzi huu wa Tanzania.” Tathmini Akizungumzia matokeo hayo Profesa Rwekaza Mkandala wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam, amesema kuwa ingawa uongozi wa CCM umekwisha sema kwamba hautaegemea kura za maoni za vyombo vya habari na taasisi nyinginezo, bado kura za maoni ni muhimu kwasababu zinaakisi mtizamo wa wapiga kura. "Tathmini hizi hawa ni watu wanaoulizwa hawaishi sayari za mbali, hawa ni wa-Tanzania wanaoishi hapa ni wananchi wa kawaida, kwa hiyo haiwezekani maoni yao yakawa tofauti kabisa na wananchi wenzao", alisema Profesa Mkandala. Kura za maoni zaidi Idhaa ya Kiswahili ya BBC inafanya mipango ya kuendelea na kura za maoni za aina mbali mbali kuhusiana na uchaguzi wa Tanzania ambao utafanyika Oktoba mwaka huu kumtafuta mrithi wa rais Benjamin Mkapa amemaliza muda wake na pia wabunge. |
| |||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
| ||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||