|
Mahakama Uswizi yaachia pesa za Mobutu
|
||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
Mahakama moja nchini Uswizi imeamuru kuwa kitita cha pesa cha Rais wa zamani wa Congo Mobutu Sese Seko ambacho kilikuwa kinazuiliwa
kwenye benki nchini humo kirudishiwe familia yake.
Familia ya marehemu Mobutu sasa inatarajia kupokea pesa hizo, zaidi ya dola milioni sita baada ya mahakama kupinga ombi lililowasilishwa na mwanaharakati mmoja la kutaka fedha hizo ziendelee kuzuiliwa na serikali au zigawiwe mashirka ya misaada. Kufuatia uamuzi huo Prof Mark Pieth ambaye alikuwa amewasilisha ombi la kutaka pesa hizo ziendelee kuzuiwa katika benki hizo nchini Uswizi amesema kuwa hii ni siku ya majonzi nchini Congo. Pesa hizo zilikuwa zinazuiliwa tangu mwaka wa '97 baada ya kifo cha Mobutu Sese Seko kufuatia madai kuwa kiongozi huyo wa zamani wa Congo na familia yake walipata utajiri huo kwa kupora mali ya umma nchini mwao. Serikali ya Uswizi ilikuwa imeweka muda wa mwisho wa kuzuia pesa hizo hadi mwezi Octoba mwaka huu. Awali serikali ya Congo ilikuwa inataka pesa hizo zirudishwe mikononi mwake ili zitumike kwa mipango ya maendeleo nchini humo lakini juhudi zake zimeambulia patupu. Rais Mobutu alitawala Zaire kwa jumla ya miaka 32, kipindi ambacho aliishi maisha ya kifahari huku wananchi wengi wakiishi kwa dhiki. Alinunua majengo mengi ya kifahari katika nchi za ulaya kando na kuwa na akaunti nyingi katika benki za nchi hizo. Baada ya serikali yake kupinduliwa na waasi waliongozwa na Laurent Kabila, babake kiongozi wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Mobutu pamoja na vibaraka wake walitoroka. Rais Mobutu alifariki nchini Morocco na hadi leo hakuna anayejua utajiri wake kamili. |
VIUNGO VYA MTANDAO WA HAPA HAPA
Shehena ya pembe haramu yanaswa Kenya 16 Juni, 2004 | Habari
Charles Taylor akemea mahakama 16 Juni, 2004 | Habari
|
||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
|
|||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||
|
|||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||||