Maisha ya waafrika Brazil

14 Julai 2014 Imebadilishwa mwisho saa 09:43 GMT

Waafrika wengi waliohamia nchini humo wanasema wanaona raha kuishi Brazil. Cha mno?
Brazil ni nchi yenye urathi mkubwa wa kiafrika , na ni kwa sababu ya historia biashara ya utumwa. Mamilioni ya watu nchii Brazil wana asili ya kiafrika. Lakini je maisha yako vipi kwa waafrika waliohamia nchini humo aidha kufanya kazi au kusoma? Mwandishi wa BBC Manuel Toledo alikuwa nchini Brazil na alikutana na baadhi yao.
Victor Macaia (katikati) na mkewe Melanito Biyouha, wanatoka nchini Cameroon. Walifungua mgahawa wao wa chakula cha kiafrika mjini Sao Paulo miaka sita iliyopita. "mwanzoni asilimia 80 ya wateja wetu walikuwa waafrika, lakini sasa asilimia 90 ni wageni na wenyeji wa-Brazil. Chakula chetu chote ni cha kiafrika,'' alisema mwanamume huyo.
"ilikuwa vigumu sana kwetu kaunza biashara hii. Wakati mwingine huna nyaraka zinazotakikana, pesa na gharama au hata uzoefu wa kazi. Inachukua muda, kufanya kazi muda wa kupitia masaibu na pia muda wa kupata faida. Lakini sasa tuko vizuri sana,'' Bwana Macaia aliongeza kusema.
Ale Fall Sow, kutoka Senegal ni mhadhiri katika chuo kikuu Brasilia. '' Nimeishi nchini Brazil kwa miaka 26. Nilikuja hapa kwa mara ya kwanza kama mwanafunzi. Mke wangu na watoto wangu ni wa-Brazil. Wanapenda Afrika na wao huenda huko kwa likizo mara kwa mara.
Nchini Brazil kuna asili mbali mbali. Kwa sababu za kihistoria, kuna watu weusi Kaskazini mwa nchi,'' asema mwanafunzi Tresor Mukendi Muteba, kutoka Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo. Nahisi kama niko nyumbani hapa. Utamaduni wa Brazil unafanana na utamaduni wa Afrika. Kwa sababu ya hilo, wakati mwingi mimi huhisi kama niko Afrika. ''
"nimekuwa nchini Brazil, kwa miezi mitatu au minne, asema Uju Juliana kutoka Nigeria. "Brazil ni mahala pazuri sana. Wanawake wa kiafrika sisi huhisi kama tuko tu nyumbani. Ningesema kwamba hapa Brazil watu huheshimu wanawake zaidi hata kuliko nchini mwangu. ''
Lacine Sanogo kutoka Ivory Coast anasema: "nilikuja hapa kucheza soka. Lakini maisha hapa ni magumu hasa kwetu raia wa kigeni. Hatupewi nafasi za kutosha, Nimekuwa nikicheza katika ligi ya daraja ya pili lakini hivi karibuni nilipata jeraha la goti. Ambavyo soka inachezwa Afrika ni tofauti sana na inavyochezwa hapa. Nimejifunza mambo mengi. ''
El Hadji Omar, kutoka Senegal anauza mali yake barabarani. "nilikuja Brazil miezi miwili iliyopita kutafuta kazi. Sijui nitakuwa hapa kwa muda gani lakini naipenda nchi hii. Kama katika sehemu nyingine yoyote duniani, kuna watu wazuri na wabaya. Lakini watu nchini Brazil ni kama tu sisi waafrika. ''
"nimekuwa hapa kwa miezi minne,'' asema Yussif Muhktar kutoka Ghana. "nilikuja hapa kufanya kazi. Wa-Brazil ni watu wazuri sana na wanapenda kila mtu na ninashukuru kwa hilo. ''
Serge Tchieguen kutoka Cameroon anasema: "ninafanya kazi ya usimamizi wa michezo, na hiyo ni sekta ambayo imekomaa sana hapa Brazil. Nimejifunza mengi. Nadhani nimebadilika na kuwa bora zaidi tangu kuja hapa miaka minne iliyopita kwa namna ambavyo nafikiria na pia kufanya kazi. ''
Ifeanyi Okafor, kutoka Nigeria, ni mhandisi katika kampuni ya kuchimba mafuta. "ninaishi eneo linaljulikana kama Macae karibu na Rio de Janeiro. Nimeishi hapo kwa miaka miwili. Ni mara ya kwanza kwangu kufanya kazi nje ya Afrika. Nimefurahi sana na nina marafiki wengi sana hapa Brazil.''