Maafa mgodini nchini Uturuki

14 Mei 2014 Imebadilishwa mwisho saa 10:38 GMT

Hitilafu ya umeme imesababisha maafa mgodini nchini Uturuki
Mlipuko ulitokea katika mgodi wa mkaa na kusababisha vifo vya watu 201 waliokuwa ndani ya mgodi huo. Wengi wamejeruhiwa vibaya
Waziri wa kawi Taner Yildiz anasema kuwa watu 787 walikuwa ndani ya mgodi huo wakati wa ajali hiyo katika mkoa wa Soma wakati hitilafu ya mtambo wa umeme iliposababisha mlipuko huo
Waokoaji walifanya kazi usiku kucha kuwatafuta manusura, lakini bwana Yildiz alisema matumaini yanadidimia ya kuweza kuwapata manusura zaidi
Jamaa na marafiki waliokuwa wamejawa hofu wamekusanyika katika mgodi huo wa kibinafsi magharibi mwa mji mkuu Ankara
Bwana Yildiz, alithibitisha idadi ya watu waliofariki na kuongeza kuwa watu 80 wamejeruhiwa.
Aliongeza kwamba kati ya wafanyakazi waliokuwa ndani ya mgodi wakati wa ajali, ni watu 360 pekee ambao wameweza kujulikana waliko ikiwemo watu waliokufa
Inaaminika kuwa gesi ya sumu ya Carbon Monoxide, ndiyo iliyosababisha vifo vingi. Gesi ya Oxygen imekuwa ikiwekwa ndani ya mgodi huo kwa mirija ili kuwaokoa wale ambao bado wamenaswa.
Hitilafu ya umeme ndiyo iliyosababisha kukatizwa kwa umeme na kuuharibu mgodi huo kabisa. Walionaswa ndani ya mgodi wanasemekana kuwa umbali wa kilomita 2 chini ya ardhi
Mlipuko ulitokea saa sita na nusu Jumanne na ripoti zinasema kuwa watu 17 walifariki ingawa idadi hiyo iliongezeka siku iliyofuata