M23: Uasi sasa basi!

5 Novemba 2013 Imebadilishwa mwisho saa 12:39 GMT

Kiguu na njia waasi wa M23 wamechukua silaha zao na kuondoka ngome zao za mwisho baada ya kushindwa na jeshi la DRC.
Shirika la misaada ya kibinadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA) linasema kuwa angalau watu 800,000 wametoroka makwao kufuatia vita kati ya serikali na waasi wa M23. Kundi hilo lilianza harakati zake dhidi ya serikali mwezi Aprili mwaka 2012.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, inasema kuwa wanajeshi wake wamekomboa ngome mbili za mwisho za waasi wa M23, Tshangu na Runyoni mapema Jumanne.
Waasi wa M23 walitoroka maeneo waliyokuwa wameyateka ya sehemu za milimani nchini DRC baada ya jeshi la serikali kukataa ombi la kusitisha vita ili kufanya mazungumzo na serikali na hata kuwaondoa kutoka katika maeneo waliyokuwa wameyadhibiti.
Jeshi la Congo liliungwa mkono na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kuwapiga waasi wa M23 Mashariki mwa DRC.
Rutshuru ni moja ya maeneo yaliyokombolewa na jeshi la serikali ya DRC, tangu mwishoni mwa wiki
Mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini ni maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini na yamekuwa kitovu cha mgogoro wa kisiasa ambao umekuwa ukitokota DRC kwa miaka mingi.