-
Kathy ana umri wa miaka 58 aliyewahi kuugua saratani ya matiti, na anaishi Cape Town, Afrika Kusini. Bado anaendelea kupatiwa matibabu ili kuhakikisha saratani hairejei tena. Picha hii ilipigwa mwaka jana baada ya kupatiwa taarifa kuwa sasa hana tena saratani. Kathy ni mtu shupavu. Nguvu yake aliipata zaidi kutokana na kuungwa mkono na mume wake, Ian na watoto wake watatu pamoja na familia yake. Picha hii imepigwa na Jeanette Verster, Marekani.
-
Zain aliwahi kuugua saratani. Anavaa riboni ya waridi na ni mwanaharakati hai wa kundi la The Hope. Wanachama wake hupita katika nyumba kuwatazama wagonjwa wa saratani, hasa wale ambao ndio kwanza wamekutwa na ugonjwa huo, kwa kuwa wanapitia wakati mgumu kipindi cha mwanzo. Wanazungumza waliyoyapitia, jinsi ya kupambana na tiba ya kemo na jinsi ya kutokata tamaa. Hawaachi kuwatembelea hata baada ya kupona, wanaendelea kuwatembelea wagonjwa na kuanzisha uhusiano wa karibu kabisa. Kundi la Hope (Matumaini) linapata msaada kutoka kwa watu wa kawaida hospitalini na pia Wakfu wa Saratani wa Saudi. Picha imepigwa na Abduljalil Al-Nasser, Saudi Arabia.
-
Abdullah Dhaim ana umri wa miaka 75, na alikutwa na saratani ya utumbo miaka kadhaa iliyopita. Madaktari waliondoa kipande cha sentimita 17 cha utumbo wake.Ana matumaini makubwa na baada ya kupona alianza kutembelea wagonjwa wengine wa saratani ili kuwaelimisha na kuwapa ari. Mke wake amekutwa na saratani ya ini hivi karibuni..... Wanawake wengi wanasema mara tu wanapokutwa na saratani, baadhi ya watu wanaacha hata kuwasalimia, kula nao pamoja na kuwa karibu yao. Baadhi ya watu nchini Saudi Arabia wanaamini saratani inaambukiza, au wanakuwa wanaogopa tu. Picha na Abduljalil Al-Nasser, Saudi Arabia.
-
Kathy Rymes (kushoto) alikutwa na saratani ya matiti mwaka 2009. Anawapa matumaini wote wenye saratani kukumbuka kuwa hawako peke yao, na kuwa kutafuta mtu wa kuzungumza naye ni muhimu wakati wa kupona. Michelle White-Malcolm (kulia) alikutwa na saratani ya matiti mwaka huo huo. Michelle anasema kuwa wagonjwa waseme jinsi wanavojisikia hasa hali ya wasiwasi ili wapatiwe msaada na watu wengine. Picha hizi zilipigwa na Scott Hussey, wa Marekani, kama sehemu ya kitabu kiitwacho Living Through Cancer (Kuishi na saratani).





































