http://www.bbcswahili.com

09 Septemba, 2008 - Imetolewa 17:59 GMT

Msafara wa basi la BBC uchaguzi Marekani

Shirika la utangazaji la Uingereza, BBC, kupitia Idhaa zake mbali mbali litafanya msafara kupitia majimbo mbali ya Marekani katika kipindi cha kampeni za uchaguzi - safari itaanza tarehe 10 Septemba huko Los Angeles na kumalizika Oktoba 17 jijini New York.

Safari hiyo itakayodumu siku 38, itaanzia katika jiji la Los Angeles kwenye pwani ya magharibi ya Marekani, tarehe 10 Septemba.Mpaka kukamilika kwake basi litakuwa limesafiri takriban kilometa 7,000 na kupitia majimbo yapatayo 15.

Basi hili la kisasa litaanza safari likiwa na waandishi 12 kutoka idhaa mbali mbali za BBC.Kila mwandishi atakuwemo kwenye safari kwa siku zisizopungua tano kabla ya kushuka na kupisha mwingine.Jumla ya waandishi 44 watakuwa wameingia na kushuka kufikia mwisho.

Waandishi wakiwemo wa redio, tovuti na televisheni, watakuwa wakifanya kazi na kulala ndani ya basi hili ambalo pia litakuwa limebeba vifaa vya kisasa vya kuandaa na kurushia matangazo kutoka sehemu yoyote wakati wa safari itakayopita katika maeneo ya vijijini pia.

Lengo la safari hii ni kuweza kupata mtizamo wa wapiga kura katika maeneo ambayo kwa kawaida waandishi wa vyombo vya kimataifa huwa hawafiki kupata maoni ya wapiga kura.Je yale yanayoandikwa na vyombo vya Marekani ndiyo yanayowagusa wananchi?Safari hii itajaribu kupata majibu.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Hassan Mhelela atajiunga na basi ifikapo tarehe 12 Oktoba katika mji wa Akron kwenye jimbo la Ohio.Kwa muda wa siku tano watakuwa njiani na kumalizia New York.Msafara utakamilika New York kwenye viwanja vya Time Square, waandishi kutoka vyombo vya Marekani kutoka ABC, NBC na CBS watawahoji waandishi wa BBC kuhusu msafara huo.