BBC navigation

UN yakosoa TZ kwa kuwafukuza wakimbizi

Imebadilishwa: 13 Septemba, 2013 - Saa 07:05 GMT

Baadhi ya wahamiaji haramu waliolazimishwa kurejea makwao na Tanzania

Umoja wa Mataifa umesema kuwa takriban wakimbizi elfu 25 kutoka Burundi wameondoshwa Tanzania kwa nguvu katika mwezi mmoja uliopita.

Afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR amesema malori yanayowasafirisha warundi yamekuwa yakivuka mpaka kila siku , huku wahamiaji haramu wengi wakikosa mahitaji muhimu kama vile maji na chakula

Katika wiki za hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikiwarejesha makwao kwa nguvu wale walioelezwa wahamiaji haramu kutoka Burundi, Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Kwa miaka mingi Tanzania iliwahifadhi mamilioni ya wakimbizi waliokuwa wakiyakimbia mapigano katika nchi jirani . Tanzania kwa upande wake inasema watu hao ni wahamiaji haramu wala sio wakimbizi.

Takriban watu milioni moja walitoroka kutoka Burundi na kuingia Tanzania wakati wa mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe wakati vita vilipozuka mwaka 1993. Wengi walirejea kwa hiari wakati amani ilipopatikana mwaka 2006.

Nchi hiyo imekuwa makao kwa mamilioni ya wakimbizi katika kipindi cha zaidi ya miaka kumi iliyopita kutokana na migogoro katika eneo la maziwa makuu.

Maafisa wa Tanzania sasa wameanza kutekeleza amri ya kuwaondoa kwa nguvu wale wanaodaiwa kuwa wahamiaji haramu kutoka Burundi, Rwanda, na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Shughuli hii imetokea wakati mmoja na mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda ambayo imekuwa ikikanusha madai ya kuchochea vurugu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mgogoro ndani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo nao unaendelea kuchochea idadi ya wakimbizi wanaotoroka vita na kuingia katika nchi jirani.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.