Tajiri atoa wito wa kuangamiza Polio

  • 29 Januari 2013
Bill Gates anafadhili miradi mingi duniani ya kupambana na ugonjwa wa kupooza

Tajiri na mhisani mkubwa duniani Bill Gates, ametoa wito kwa dunia kuhakikisha kuchukua nafasi ya kuangamiza kabisa ugonjwa wa kupooza.

Katika mahojiano na BBC, Gates mmiliki wa kampuni kubwa zaidi ya kutengeza programu za komputa, na ambaye wakfu wake hutoa msaada kwa miradi ya kumaliza Polio, alisema kuwa utakuwa kama muujiza ikiwa ugonjwa huo utaangamizwa.

Alitoa mfano wa ugonjwa wa Tetekuwanga ulivyoangamizwa kabisa na kuzitaka nchi kuweka juhudi kuhakikisha kuwa nao Polio unaangamizwa.

Huku ugonjwa huo ukiwa bado ni tatizo kubwa nchini Pakistan, Nigeria na Afghanistan, Gates alisema kuwa sharti pawepo msisitizo kuwa chanjo inaokoa maisha.

Maafisa kadhaa wa afya wameuawa Pakistan kwa kushiriki kampeini ya kupambana na Polio

Wakati huohuo, afisaa mwingine aliyekuwa anashiriki katika kampeini ya kutoa chanjo dhidi ya Polio nchini Pakistan ameuawa akiwa ni wa kumi kuuawa zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Alikuwa polisi aliyekuwa anatoa ulinzi kwa maafisa wa chanjo. Wanamgambo wa Taliban, wanapinga kabisa kutolewa kwa chanjo dhidi ya Polio.