bbc.co.uk navigation

Ajilipua katika kambi ya jeshi Nigeria

Imebadilishwa: 7 Februari, 2012 - Saa 18:14 GMT
Nigeria

Boko Haram wamekuwa wakifanya mashambulio mengi


Mtu mmoja aliyevaa nguo za kijeshi amejilipua nje ya kambi ya jeshi katika jiji la Kaduna nchini Nigeria, huku kukiwa na taarifa za mashambulio mengine, maafisa wanasema.

Msemaji wa jeshi amesema wanajeshi walimpiga risasi lakini alifanikiwa kulilipua bomu katika gari alilokuwa akiendesha.

Kumekuwa na milipuko pia katika kambi ya jeshi la anga jijini humo, wanasema wafanyakazi wa shughuli za dharura, huku wakazi wakisema kulikuwa na mlipuko mwingine karibu na daraja moja.

Wanamgambo wa Kiislam wameua mamia ya watu kaskazini mwa Nigeria.

Siku ya Jumatatu usiku, kulikuwa na majibizano ya risasi kati ya wanajeshi na watu wanaodhaniwa kuwa ni wanamgambo mjini Kano, ulipo pia kaskazini.

Mlipuko huo umetokea katika kambi ya jeshi la Nigeria mjini Kaduna.

"Mlipuaji wa kujitoa mhanga ndio mtu pekee aliyekufa," amesema msemaji wa jeshi Meja Jenerali Raphael Isa.

Mwandishi wa BBC mjini Kaduna amesema aliona magari matatu ya kubebea wagonjwa yakiondoka katika kambi hiyo kuelekea katika hospitali ya mjini humo.

Kundi la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulio kadhaa katika eneo hilo kujaribu kuiondoa serikali ya taifa na kuanzisha taifa la Kiislam.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2012 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.