Kupambana na ukame pembe ya Afrika

Imebadilishwa: 20 Januari, 2012 - Saa 16:29 GMT

Kupambana na ukame pembe ya Afrika

  • Ukame unazidi kutishia maisha ya watu takriban milioni 13 wanaoishi pembe ya Afrika na wengi wanaendelea na maisha ya uchungaji. Alejandro Chaskielberg amefika eneo hilo na shirika la Oxfam ambao wana miradi mbalimbali ya kutoa misaada inayowasaidia wale wenye shida.
  • Miongoni mwa miradi hiyo ni Oxfam kushirikiana na akina mama, likiwasaidia kulea familia zao kwa kupembejea ardhi itakayowawezesha kulima.
  • Miradi ya kutengeneza bustani inatarajiwa kuanza katika vijiji vitatu maeneo ya kaskazini mwa Turkana. Elisabeth anaishi na watoto wake wanane na anaihudumia familia yake mwenyewe tangu mumewe alipofariki. Alisema: "Ninashukuru sana kwa uchungaji lakini wanyama siku hizi hawawezi kuhimili hali. Kukiwa na ukame, wanyama wako hufa nawe unabaki bila kitu. Kama ningeweza kufanya jambo moja basi ningependa niwe na biashara yangu mwenyewe na kuweza kupata kipato."
  • Viwanja vya umwagiliaji ni mfano mmoja tu wa hatua za mapema za kupambana na athari ya ukame. Ripoti ya pamoja ya Oxfam na Save the Children ilisema taarifa kuhusu ukame huo uliokithiri eneo hilo ulitakiwa kutolewa mapema.
  • Ripoti hiyo imeongeza kuwa jumuiya za kimataifa na serikali lazima zifanye mabadiliko sasa, ikishinikiza kuwa hatari hiyo lazima idhibitiwe.
  • Selina Napete ni mmoja waliofaidika kutokana na mpango huo wa Oxfam: "Inapokuwa hainyeshi vyanzo vya maji hukauka, matunda hayaivi na wanyama hufa. Hakuna kikubwa unachoweza kufanya ili kuishi. Tulikuwa tukila mara moja kwa siku na watoto wangu walikuwa wakilia kwasababu ya njaa. Nilipoanza bustani ya mboga za majani niliweza kuanza kuwalisha wanangu. Naweza kutumia pesa nilizopata kutokana na mauzo ya mboga hizo kuwapeleka shule na kuwanunulia vitabu.
  • John anaishi karibu na kijiji cha Lomekui ziwa Turkana pamoja na wake zake wawili na watoto 10. Kwa asili ni mchungaji lakini amepata tabu wakati wa ukame. Wanyama wake wengi wamekufa, huku akipata tabu ya kuilisha familia yake. John alipewa ngamia wanne na mbuzi 20 kama sehemu ya mpango wa Oxfam. Alisema: Ni changamoto kubwa kuishi hapa na ukame huu, mifugo haitoi chochote siku hizi na sina namna ya kufanya. Nakumbuka nilicheka sana Oxfam waliponipa ngamia. Katika siku za usoni nataka niongeze idadi ya ngamia na mbuzi."
  • Picha za Alejandro Chaskielberg zimechukuliwa kwa kutegemea mwanga wa mbalamwezi na taa.

bbc.co.uk navigation

BBC © 2012 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.